Urusi na Ukraine zaendelea kupambana vikali huko Kursk
14 Agosti 2024Baada ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kusema kuwa vikosi vyake vinaendelea kusonga mbele katika mkoa huo wa Kursk , wizara ya ulinzi ya Urusi imesema katika taarifa yake kwamba imezuia majaribio ya kusonga mbele ya vikosi vya Ukraine katika maeneo matano ndani ya ardhi ya Urusi.
Awali, Ukraine ilisema inadhibiti maeneo 74 ya makaazi katika mkoa huo wa Kursk wa Urusi, na ilikuwa inaendelea kusonga mbele. Wanablogu wameandika kuwa Urusi inapambana vikali huko Kursk huku Moscow ikisema kwamba Ukraine ilishambulia kwa droni zaidi ya 100.
Soma pia: Rais wa Ukraine amesema majeshi yake yamesonga mbele katika jimbo la Kursk
Kamanda mkuu wa jeshi la Ukraine, Oleksandr Syrskyi, amesema mji wa Sudzha huko Kursk ambao ni kitovu cha usafirishaji wa gesi asilia ya Urusi kuelekea Ulaya kupitia Ukraine, ulikuwa chini ya udhibiti kamili wa jeshi la Ukraine na kwamba shughuli ya usambazaji wa gesi ilikuwa inaendelea hii leo kama kawaida.
Waziri wa Ulinzi wa Lithuania Laurynas Kasciunas amesema hivi leo kwamba Urusi inawahamisha baadhi ya wanajeshi wake kutoka eneo la Baltic la Kaliningrad ili kukabiliana na uvamizi wa Ukraine katika mkoa wa Kursk. Kaliningrad imepakana na Poland na Lithuania ambazo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya na jumuiya ya kujihami ya NATO.
Zelensky afanya mkutano kujadili hali huko Kursk
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema hivi leo kuwa amefanya mkutano kuhusu hali jumla katika eneo la Kursk na kutathmini iwapo itahitajika kuwekwa kwa muda utawala wa kijeshi ili kuimarisha usalama na kupanga mikakati ya kuwasilisha misaada ya kibinadamu.
Soma pia: Urusi, Ukraine mambo yazidi kuwa mabaya
Oleksandr Syrskyi, Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Ukraine amesema:
"Vikosi vya Ulinzi vinaendelea na operesheni ya mashambulizi kwenye eneo la mkoa wa Kursk. Kuanzia leo, askari wanasonga mbele kwa karibu kilomita 1 hadi mbili katika baadhi ya maeneo. Tumekamilisha zoezi la kuwasaka na kuwaangamiza maadui kwenye eneo la Sudzha (Suja). Kuanzia asubuhi ya leo tumewakamata zaidi ya askari mia moja wa jeshi la adui."
Serikali mjini Kyiv imesisitiza kuwa nia yake ni kuyalinda maisha ya watu wake na si kulikalia eneo hilo, na pia itaamuru kuwepo kwa ukanda salama huko Kursk ili kuwezesha uhamisho wa raia wanaotaka kuelekea Urusi au Ukraine.
Soma pia: Hali ya hatari yatangazwa kwenye jimbo la Belgorod
Maelfu ya wanajeshi wa Ukraine walivamia eneo la mpakani mnamo Agosti 6 hadi kuwasili katika eneo hilo la magharibi mwa Urusi la Kursk, katika kile rais Putin alisema ni uchochezi mkubwa unaolenga kuweka mizani ya nguvu kwenye uwezekano wa mazungumzo ya kusitisha mapigano.
Mbunge wa Urusi Maria Butina amesema nchi za Magharibi zinahusika katika uvamizi huu wa Ukraine katika ardhi ya Urusi huku akisema kuwa hatua hiyo ni sawa na "kumuamsha simba aliyelala".
Marekani na nchi zingine za magharibi zinazoiunga mkono Ukraine zilikanusha kuwa na taarifa zozote kabla ya mashambulizi makubwa ya Ukraine kwenye eneo la Urusi la Kursk.
(Vyanzo: AP, DPAE, Reuters, AFP)