1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki, Saudi Arabia walaani msimamo wa Taliban

Hawa Bihoga
22 Desemba 2022

Uturuki na Saudi Arabia yamekuwa mataifa ya kwanza yenye idadi kubwa ya waislamu kulaani uamuzi wa Taliban kuwapiga marufuku wanawake kujiunga na vyuo vikuu, huku maandamano Afganistan yakushuhudiwa kupinga uamuzi huo

https://p.dw.com/p/4LKXA
Rumänien Bukarest | Treffen der NATO-Außenminister | Mevlut Cavusoglu, Türkei
Picha: Andreea Alexandru/AP Photo/picture alliance

Uturuki na Saudi Arabia yamekuwa mataifa ya kwanza yenye idadi kubwa ya waislamu kulaani vikali uamuzi wa mamlaka ya Taliban kuwapiga marufuku wanawake kujiunga na vyuo vikuu, wakati ambapo idadi ya wanawake kadhaa wakiingia mitaani kuandamana kupinga hatua hiyo mjini Kabul leo Alhamis.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu, amesema uamuzi huo wa Taliban sio wa kiislamu na wala haujazingatia misingi ya kibinadamu.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari akiwa na mwenzake wa Yemen Ahmad Awad bin Mubarak, Cavusoglu ametoa wito kwa watawala hao wa Afghanistan kubadili uamuzi huo.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Uturuki amehoji kwa mamalaka ya Taliban kuna madhara gani endapo wanawake nchini humo watapata haki yao ya elimu?

Soma zaidi:Taliban yazuia wanawake kujiunga na vyuo vikuu

Ameendele kuweka bayana kwamba hakuna maelezo katika dini ya kiislamu inayopinga elimu kwa wanawake na kinyume chake dini hiyo inahimiza elimu na sayansi.

 "Tunakata marufuku hiyo iondolewe, hatuoni kama ni sawa." Alisema waziri huyo wa Uturuki.

Aidha ameongeza kwamba tumaini lao ni Taliban kuachana na uamuzihuo ambao utawagharimu mamilioni ya wasichana nchini humo.

"Tunazungumzia juu ya wanafunzi wa kike wapatao milioni moja ambao wanaweza kwenda chuo kikuu. Kuna madhara gani juu ya elimu kwa wanawake? Kuna madhara gani kwa Afghanistan kutekeleza?" Alihoji katika mkutano huo wa wanahabari.

Saudi Arabia: Mataifa ya kiislam  yashangazwa na uamuzi huo

Saudi Arabia ambayo hadi mnamo mwaka 2019 ilikuwa ikitekeleza vikwazo kadhaa dhidi ya wanawake ikiwemo wanawake kusafiri, masuala ya ajira na mambo mengine muhimu katika maisha ya kila siku ikiwemo kuendesha gari, nayo imeungana na Uturuki kukosoa msimamo huo wa serikali ya Taliban.

Afghanistan | Frauendemonstrationen in Kabul
Makundi ya wananwake wakiandamana kwenye mitaa mjini Kabul leo AlkhamisiPicha: privat

Wizara ya mambo ya nje ya Saudi Arabia katika taarifa yake ya jana Jumatano ilioneshwa kushangazwa na uamuzi huo wa Taliban.

Taarifa hiyo iliweka bayana namna ambavyo mataifa mengi ya kiislam yamestajabishwa na uamuzi huo unaokiuka kundi la wasichana na wananwake.

Soma zaidi:Wanawake Afghanistan waandamana mjini Kabul

Hapo awali, Qatar, ambayo ilishirikiana na mamlaka ya Taliban, pia alilaani uamuzi huo ambao unaonesha taswira halisi ambavyo haki za wanawake zinavyokiukwa katika taifa hilo.

Upinzani dhidi ya kauli hiyo nchini Afganistan

Uamuzi huo wa Taliban umekutana pia na upinzani mkali kutoka jumuiya ya kimataifa na mataifa ambayo yana idadi kubwa ya waislam.

Katika ishara nyingine ya upinzani wa ndani, wachezaji kadhaa wa Kriketi wa Afghanistan wamelaani marufuku hiyo.

Kriketi ni mchezo maarufu nchini humo nawachezaji wana mamia kwa maelfu ya wafuasi ikiwemo kwenye mitandao ya kijamii.

Katika kile kinachoonekana kuendelea kupinga msimamo huo, makundi ya wanawake leo Alkhamisi yamejitokeza kwenye mitaa mjini Kabul kulaani juu ya uamuzi huo wa Taliban uliotolewa mapema wiki hii.

Soma zaidi:Guterres aitaka Taliban kuruhusu wasichana kusoma

Mmoja wa wanawake waandamanaji amekaririwa na shirika la habari la Associated Press akisema vikosi vya usalama vya Taliban vilitumia nguvu katika kuyatawanyamakundi ya wanawake huku wengine wakikamatwa.

Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kuwa wanafunzi wa kiume katika vyuo mbalimbali wamesusia kufanya mitihani hadi hapo wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu watakaporejeshwa.