Viongozi wa Chadema waachiliwa kwa dhamana
24 Septemba 2024Viongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania Chadema, waliokamatwa jana na jeshi la polisiwakidaiwa kuhamasisha maandamano yaliyopangwa kufanywa na Chama hicho, wameachiwa huru na kutakiwa kuripoti polisi Septemba 30 mwaka huu, huku wadau wa Habari wakilaani jeshi la polisi kukamata wanahabari na kulitaka kuheshimu majukumu ya wanahabari wanapotimiza wajibu wao. Florence Majani ametuandalia ripoti hiyo.
Viongozi hao wakuu wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti Bara, Tundu Lisuu, Mwenyekiti kanda ya Kaskazini, Godbless Lema waliachiwa jana usiku kwa dhamana na kutakiwa kuripoti tena polisi Septemba 30.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Viongozi hao pamoja na watu wengine 14, walikamatwa jana kwa madai ya kukaidi katazo la maandamano, uchochezi na kuhamasisha maandamano yaliyopangwa kufanyika jana kama hatua ya kuishinikiza serikali kuchukua hatua stahiki baada ya kuwepo kwa mfululizo wa matukio ya mauaji na utekaji.
Wakili wa Chadema, Hekima Mwasipu, ameiambia DW kuwa "baada ya kuandika maelezo hayo, wakapata dhamana, usiku mida ya saa 4. Nashukuru Mungu walitoka wote baada ya kupata dhamana".
Soma: Chadema yaikosoa serikali baada ya kuteswa kwa viongozi wake
Pamoja na viongozi wa Chadema waandishi wa Habari wa hapa nchini, kadhalika walikamatwa jana wakati wakiwa katika maeneo ambayo jeshi la polisi liliweka kambi kusimamia ulinzi na usalama dhidi ya mpango wa maandamano hayo ya Chadema.
Waandishi waliokamatwa ambao hata hivyo baadaye waliachiwa, ni Mariam Shabani wa EATV, Michael Matemanga na Lawrence Mnubi wa Mwananchi pamoja na Jennifer Gila wa Nipashe.Rais wa Tanzania aamuru uchunguzi visa vya utekaji na mauaji
Mariam Shaban, ni mwanahabari wa kituo cha Televisheni cha EATV, na mwathirika wa kamatakamata hiyo na anasema baada ya kukamatwa hawakuambiwa kosa bali vifaa vyao vilikaguliwa na kisha kuachiwa. "kuna muda walikuwa wanatuuliza tu, jina lako, mwandishi wa chombo gani, hivyo, wakachukua karatasi wakatushikisha hivi, wakatupiga na picha, sasa sijui zilikuwa zinaenda wapi, ila hicho kitu kimefanyika pia."
Wadau wa sekta ya Habari wamelaani kitendo hicho cha kuwakamata wanahabari hao na kulitaka jeshi la polisi kusema vitendo hivyo si afya kwa taifa. Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile amesema "kuwakamata waandishi wa Habari si sawa hata chembe, na tunaomba hili lisirudie, tutafanya utaratibu, tutazungumza na viongozi wakuu wa polis, ili tunakolekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ili haya mambo yasitokee , tukajikuta tena katika sintofahamu, ambayo haitupi afya kama taifa."
Soma ripoti hii: Polisi yamtia mbaroni kiongozi maarufu wa upinzani Tanzania
Chadema ilitangaza mpango wake wa maandamano ya nchi nzima mnamo Septemba 11 wakiishinikiza serikali kuwajibika baada ya kuwepo kwa mfululizo wa matukio ya utekaji na mauaji ya raia na baadhi ya makada wa Chadema.
Maandamano hayo, waliyoyaita ya maombolezo na amani, yalipangwa kufanyika jana Septemba 23, lakini jeshi la Polisi, liliweka ulinzi mkali, Katikati ya jiji la Dar es Salaam na viunga vyake huku baadhi ya viongozi wa chama hicho na wanahabari wakiwekwa rumande.