1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa Mursi waitisha maandamano mengine

Admin.WagnerD29 Julai 2013

Wafuasi wa Rais aliyeng'olewa madarakani nchini Misri Mohammed Mursi wameitisha maandamano mengine huku mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa ulaya Catherine Ashton akitarajiwa kufanya mazungumzo na serikali na upinzani

https://p.dw.com/p/19FjW
Picha: Reuters/Mohamed Abd El Ghany

Muungano wa makundi ya kiislamu yanayopinga kung'olewa madarakani kwa Mursi umewahimiza wafuasi wao kuandamana katika majengo ya asasi za kiusalama leo usiku na kuitisha maandamano mengine hapo kesho yanayolenga watu milioni moja kujiunga nayo.

Muungano huo wa kupinga mapinduzi ya kijeshi umewataka wamisri kujitokeza na kuandamana katika mabarabara na mitaani kurejesha kile ulichokitaja uhuru wao na hadhi ambayo inakiukwa na mapinduzi hayo na pia kutetea haki ya mashujaa waliouawa kwa kupigwa risasi.

Wafuasi wa Mursi waonywa

Taarifa hiyo kutoka kwa wafuasi wa Mursi inakuja siku moja baada ya baraza la ulinzi wa kitaifa linalojumuisha Rais wa muda anayeungwa mkono na jeshi na mkuu wa jeshi kuonya kuwa itachukua hatua kali dhidi ya waandamanaji iwapo watapitiliza mipaka yao ya kuwa na haki ya kuandamana kwa amani.

Hali ya wasiwasi ingaali imetanda nchini humo baada ya watu 72 kuuawa katika maandamano ya kumuunga mkono Mursi siku ya Jumamosi.Huku mzozo huo ukipamba moto, mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Catherine Ashton anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi kadhaa wa serikali na wa upande wa upinzani.

Mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Bi Catherine Ashton akutana na Rais wa muda wa Misri Adli Mansour
Mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Bi Catherine Ashton akutana na Rais wa muda wa Misri Adli MansourPicha: picture-alliance/dpa

Anatarajiwa kukutana na Rais wa muda Adli Mansour na makamu wa rais aneyeshughulikia masuala ya kigeni Mohammed El Baradei pamoja na wanachama wa udugu wa kiislamu na vuguvugu la Tamarod liliondaa maandamano makubwa yaliyomng'oa madarkani Mursi.

Jumiya ya kimataifa ina wasiwasi

Katika taarifa, Ashton amesema ataitisha kuwepo kwa kipindi cha mpito kinachojumisha kila pande husika ikiwemo chama cha udugu wa kiislamu na kukariri wito wake wa kusitishwa kwa ghasia.

Tawi kisiasa la udugu wa kiislamu,chama cha uhuru na haki kimethibitisha kitakutana na Ashton hii leo kwa misingi ya uhalali wa kikatiba na kwa lengo la kumaliza mapinduzi ya kijeshi.Udugu wa kiislamu umesisitiza kuwa hautakubali suluhu lolote ambalo halitahusisha kurejeshwa madarakani kwa Mursi.

Mfuasi wa Mohammed Mursi abeba bango la picha yake mjini Cairo
Mfuasi wa Mohammed Mursi abeba bango la picha yake mjini CairoPicha: Reuters/Mohamed Abd El Ghany

Umwagikaji huo wa damu katika taifa hilo la kiarabu lenye idadi kubwa ya raia limezua hali ya wasiwasi kutoka kwa jamii ya kimataifa huku katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban ki Moon akiwaonya viongozi wa muda nchini Misri kuwa kila kifo kinachotokea nchini humo kinaufanya mzozo huo kuwa mgumu kuutatua.

Wafuasi wa Mursi wamepania kuendelea na mapambano huku maelfu wakiwa bado wamepiga kambi katika uwanja wa Rabaa al Adawiya palipozuka ghasia za Jumamosi.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman