1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

MSF: Hali ya kiutu Sudan ni ya kutisha

Angela Mdungu
12 Oktoba 2024

Shirika la kutoa misaada la Madaktari wasio na Mipaka la MSF limeelezea wasiwasi wake kuhusu hali inayowakabili watu wa Sudan na kuzitolea wito pande hasimu za mzozo huo ziruhusu misaada ya kiutu.

https://p.dw.com/p/4liKG
Kambi ya wakimbizi ya Zamzam, Sudan
Raia wa Sudan waliolazimika kuyahama makazi yao wakiwa katika kambi ya wakimbizi ya ZamzamPicha: Karel Prinsloo/AP/picture alliance

Wafanyakazi wa shirika hilo wameizungumzia hali ya Sudan wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini humo vikisababisha ongezeko kubwa la utapiamlo na njaa.

Maeneo yenye mizozo hayafikiki kwa urahisi. Kwa Sudan, Shirika la Madaktari wasio na Mipaka la MSF ni miongoni mwa mashirika machache ya kimataifa ambayo bado yanaweza kufanya shughuli zake nchini humo.

Wakati lilipotoa taarifa yake jijini Nairobi, MSF lilisema kuwa, watu milioni 26 karibu sawa na nusu ya idadi jumla ya watu wa Sudan wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Katika taarifa hiyo mratibu wa shirika hilo Claire San Filippo, alielezea hali ya utapiamlo nchini humo kuwa ni ya kuogofya.

Soma zaidi: Kilicho nyuma ya vita ambacho kinasababisha njaa Sudan

Alitolea mfano wa mwanamke mmoja mwenye watoto watatu ambaye ameshawapoteza wanafamilia 8 kutokana na mzozo huo. Aliyakimbia machafuko katika mji wa El-Fasher huko Darfur na alielezea kuwa mauaji na vita viko kila mahali. Ilimchukua mwanamama huyo mwezi mmoja kutoka kwenye mji huo hadi kufika katika kambi ya wakimbizi mashariki mwa Chad.

Wakimbizi wa Sudan waliokimbilia Adre, Chad
Wakimbizi wa Sudan nje ya hospitali wakisubiri huduma ya madaktari wa MSF mjini Adre nchini Chad.Picha: Mohammad Ghannam/MSF/REUTERS

Kulingana na Mratibu wa MSF, Shirika hilo limeshaandikisha visa vya utapiamlo wa kiwango cha juu vya asilimia 32 ya watu wanaoishi kwenye kambi ya Zamzam Kaskazini mwa Darfur na huko Nyala Darfur Kusini.

Kutokana na vizuizi, MSF ililazimika kufanya uamuzi wa kusikitisha wa kusitisha shughuli za utoaji wa chakula katika kambi ya Zamzam mahali ambapo pametangazwa kuwa kuna baa la njaa

MSF yasitisha huduma huku kukiwa na upungufu mkubwa wa mahitaji

Mratibu wa madaktari wasio na mipaka Claire San Filippo amesema wakati kukiwa na upungufu mkubwa wa mahitaji, hawakuwa na namna zaidi ya kusitisha shughuli ya kuwahudumia watoto 5,000.   

San Fillipo ameelezea pia namna vituo vya afya vinavyosaidiwa na MSF katika mji mkuu Khartoum na El-Fasher vilivyoporwa, kutekwa, na kushambuliwa mara kadhaa. Wahudumu wa afya katika maeneo hayo wamekuwa wakinyanyaswa na kushambuliwa.

Mmoja wa watoa huduma za afya Lisa Searle aliyefanyakazi kwa miezi minne Khartoum anasema anakumbuka namna siku moja majira ya ya saa tisa au kumi alfajiri aliamshwa na milio ya risasi.

Watoto wa Sudan wanakabiliwa na Utapiamlo
Mmoja wa watoto wa Sudan akipatiwa matibabu na daktari wa shirika la MSF katika kambi ya wakimbizi ya Metche nchini ChadPicha: Patricia Simon/AP Photo/picture alliance

Anaongeza kuwa wimbi jipya la machafuko limewashtusha na kuwaogopesha raia na amesisitiza kwamba wafanyakazi wenzake ambao ni raia wa Sudan wanakabiliwa na hofu waliyonayo watu wanaowasaidia.

Soma zaidi: Wasudani wamenasa kwenye ukatili, njaa na maradhi

Mgogoro kati ya wanamgambo wa kundi la RSF chini ya  Mohamed Hamdan Daglo na jeshi linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan umewauwa maelfu ya watu tangu machafuko yalipoanza mwezi Aprili mwaka uliopita. Mzozo huo umepelekea maelfu ya watu kulazimika kuyahama makazi yao.

Kikosi cha RSF na jeshi ambao ni mahasimu katika vita hivyo wamekuwa wakituhumiwa kwa kufanya ukatili katika vita hivyo ikiwa ni pamoja na kuwalenga raia, kufanya mashambulizi katika makazi ya watu bila kujali, uporaji na kuzuia misaada.