1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Waziri Mkuu Cambodia kumrithisha madaraka mwanaye?

David Hutt Iddi Ssessanga
23 Julai 2023

Akiwa madarakani kwa takriban miaka 40, Waziri Mkuu wa Cambodia Hun Sen ndiye kiongozi aliyekaa muda mrefu zaidi barani Asia. Anatarajiwa kudumisha utawala wa nasaba kwa kumuachia mwanawe uwaziri mkuu katika uchaguzi.

https://p.dw.com/p/4UHZn
Vor den Parlamentswahl in Kambodscha Hun Manet
Picha: Heng Sinith/AP/dpa/picture alliance

Cambodia imepiga kura siku ya Jumapili huku Waziri Mkuu aliyeko madarakani Hun Sen akihakikishiwa kushinda baada ya kukandamiza aina zote za uasi na upinzani. Kura hiyo iliashiria mabadiliko ya uongozi wa mara moja baada ya kizazi kzima ambapo chama tawala cha Cambodian People's Party (CPP) kinatarajiwa kuzoa viti vya vingi vya ubunge.

Baada ya mpinzani mkuu wa CPP kuzuiwa kushiriki katika kura hiyo kutokana na hoja ya kiufundi ya usajili, wachambuzi wengi wanasema kura hiyo ya upande mmoja itatumika kama kura ya moja kwa moja kuidhinisha mipango ya Waziri Mkuu Hun Sen kukabidhi madaraka kwa mwanawe mkubwa, Hun Manet, ambaye anaongoza jeshi la nchi hiyo.

Soma pia: Kiongozi wa upinzani Cambodia afungwa miaka 27 jela kwa uhaini

Inawezekana kwamba kabla ya mwishoni mwa Agosti, mabadiliko ya uongozi yanaweza kushuhudia karibu baraza lote la mawaziri likibadilishwa kwa kuingiza maafisa vijana, wengi wao wakiwa watoto au jamaa wa vigogo wa chama tawala wanaozeeka. Baadhi ya wataalamu wanaona kuwa makabidhiano ya Hun Sen ya uwaziri mkuu yanaweza kufanyika kwa wakati mmoja.

Urithi wa kizazi

Chama cha CPP kilichukua madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 1979 baada ya waasi wa kundi la Khmer Rouge, akiwemo Hun Sen, kurejea pamoja na jeshi la Vietnam kupindua utawala wa mauaji ya halaiki. Hun Sen aliteuliwa kuwa waziri mkuu mwaka 1985, na kumfanya kuwa kiongozi wa serikali aliyeongoza kwa muda mrefu zaidi duniani.

Cambodia I Hun Manet
Hun Manet, katikati, mwana wa Waziri Mkuu wa Cambodia, Hun Sen, pia mkuu wa jeshi, akipokea bendera ya Chama cha Watu wa Cambodia kutoka kwa baba yake na Waziri Mkuu Hun Sen, juu kulia, wakati wa sherehe za kampeni za uchaguzi wa chama mjini Phnom Penh Cambodia, Jumamosi, Julai 1, 2023.Picha: Heng Sinith/AP/picture alliance

Pamoja na Hun Manet kurithi uwaziri mkuu wa babake, inatarajiwa pia kuwa watoto wa waziri mwenye nguvu wa mambo ya ndani, Sar Kheng, na waziri wa ulinzi Tea Banh pia watarithi nafasi za baba zao.

Hadi theluthi mbili ya baraza la mawaziri, linaweza kutoa nafasi kwa maafisa vijana, wakati manaibu waziri mkuu na mawaziri wengi wasio na wizara maalum pia watafanyiwa mabadiliko, kulingana na orodha za wateule wa ndani zilizovuja mapema mwaka huu.

Kwa hivyo uchaguzi huo unaweza kusababisha kurudiwa kwa historia. Katika uchaguzi mkuu uliopita wa 2018, CPP ilishinda viti vyote 125 vya ubunge baada ya kukifuta kwa lazima chama kikuu cha upinzani wakati huo. Chama cha Kitaifa cha Uokoaji cha Cambodia (CNRP) kilipigwa marufuku kwa madai ya uwongo ya kupanga mapinduzi yaliyoungwa mkono na Marekani.

Mwezi Mei mwaka huu, kufuatia miezi kadhaa ya vitisho kwa wanachama wake wakuu, mpinzani pekee wa kuaminika wa CPP, chama  cha Candlelight Party, kilizuiwa kushiriki katika uchaguzi wa Jumapili kwa sababu ya mzozo wa makaratasi - uamuzi ambao Amnesty International ilisema "ulichochewa kisiasa."

Chama cha Candlelight - ambacho kilipata asilimia 22 ya kura za wananchi katika uchaguzi wa mitaa wa mwaka jana - kilidai kuwa huu ulikuwa uamuzi wa uwongo.

Tangu mwanzoni mwa mwaka, mamlaka imefunga vyombo huru vya habari, kuwafunga wanaharakati wengi wa upinzani na wakosoaji, na kuanzisha matihani ya uaminifu katika jamii zote. Kwa makadirio, zaidi ya wanachama 6,000 wa vyama vya upinzani wamehamia CPP - ama kwa woga, motisha za kifedha au hamu ya maisha ya utulivu.

Kambodscha | Premierminister Hun Sen
Hun Sen, mtawala wa muda mrefu wa Cambodia na aliyekuwa mpiganaji wa msituni wa Khmer Rouge, anatimiza umri wa miaka 71 mwezi Agosti.Picha: Heng Sinith/AP Photo/picture alliance

"Uchaguzi wa Jumapili unafanana kidogo na mchakato halisi wa kidemokrasia," Human Rights Watch ilisema katika taarifa wiki hii. Hun Sen hajaacha lolote lile kama sehemu ya mchakato mpana wa urithi wa vizazi ambao utashuhudia wanachama vijana wakirithi mikoba ya kutawala nchi ambayo wastani wa umri ni miaka 26 tu.

Siku ya makabidhiano

Lakini Sam Seun, mchambuzi wa sera katika Chuo cha Kifalme cha Cambodia, alisema alitarajia Hun Sen kusalia kama waziri mkuu hadi angalau 2025, kusimamia kizazi kipya cha mawaziri, ambao wengi wao wana umri wa miaka 40. Ikiwa mabadiliko hayo yataeenda vizuri, basi Hun Sen atajiuzulu na kumpa mtoto wake mkubwa, Seun alitabiri.

"Miaka mitatu iliyosalia kabla ya uchaguzi wa 2028 itakuwa mtihani kwa uongozi wa Hun Manet ikiwa ataweza kushinda uchaguzi wa jumapili au la," aliongeza. Hun Manet aliteuliwa kuwa mkuu wa jeshi na naibu kamanda mkuu wa jeshi lote mnamo 2018.

Tangu wakati huo Manet mwenye umri wa miaka 45 ameendelea kuongoza tawi la vijana la chama tawala na mashirika yake kadhaa ya "kibinadamu". Mwishoni mwa 2021, chama kilimkubali kama mgombeaji wake wa baadaye wa uwaziri mkuu.

Hata hivyo, hajawahi kushika wadhifa wa kuchaguliwa wala nafasi katika serikali, na kuibua maswali kuhusu uzoefu wake.

Kambodscha | Parlament
Wapiga kura wameachwa bila chaguo ila kukikabidhi chama cha Hun Sen cha Cambodian People's Party (CPP) kura nyingi katika bunge lenye wabunge 125.Picha: De Ratha/Cambodia National Assembly/AFP

Majibu ya Magharibi

Jambo lingine lisilojulikana ni jinsi demokrasia za Magharibi zitakavyojibu. Uhusiano wao na Kambodia umezidi kuwa mbaya tangu Phnom Penh ilipochukuwa mwelekeo wa kimabavu baada ya 2017 na pia kwa sababu ya urafiki wake wa karibu na China.

Wachambuzi wengi wanaona kuwa nchi za Magharibi zitachukua mtazamo wa kusubiri na kuona, zikitumai kwamba utawala wa Hun Manet ambao haujaundwa kikamilifu hatimaye utashiriki katika maelewano na mataifa ya Magharibi ambayo Phnom Penh amedai kimakosa kuwa imeutafuta kwa miaka mingi.

"Marekani na Umoja wa Ulaya zitakaribisha fursa ya kufanya kazi na damu mpya, bila shaka," alisema Sophal Ear, msaidizi mkuu na profesa katika Chuo cha mafunzo ya usimamizi ya Thunderbird kilichoko Arizona.

"Lakini," aliongeza, "natumai haitachukua miaka 38 zaidi kabla watambue kuwa kuna kitu kibaya katika 'demokrasia' ya Cambodia."