1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Ukraine ajiuzulu

25 Julai 2014

Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk alitangaza kujiuzulu jana jioni, baada ya muungano wa vyama vilivyounda serikali yake kusambaratika. Hatua hiyo inazidisha changamoto kwa nchi yake inayokabiliwa na mizozo mingi.

https://p.dw.com/p/1Cikr
Waziri Mkuu wa Ukraine aliyejiuzulu, Arseniy Yatsenyuk
Waziri Mkuu wa Ukraine aliyejiuzulu, Arseniy YatsenyukPicha: picture-alliance/dpa

Katika tangazo la kujiuzulu kwake ambalo lilikuja bila kutegemewa, Arseniy Yatsenyuk alisema ameichukua hatua hiyo baada ya kuvunjwa moyo na bunge la mseto wa vyama, na pia kuzuiliwa kwa juhudi za serikali yake baada ya vyama kadhaa kujiondoa katika muungano uliounda serikali hiyo. Yatsenyuk alisema bunge limeishiwa uwezo wa kutimiza majukumu yake ili kuimarisha uchumi na kuendeleza vita dhidi ya waasi wa mashariki wanaotaka kujitenga.

''Nitawezaje kesho kununua mafuta ya vifaru vinavyotumiwa vitani, nitalipa vipi fidia kwa familia za wanajeshi wanaouawa, nitalipaje mishahara ya wanajeshi? Vyama vilivyojiondoa serikalini vimecheza karata ya maslahi yao kisiasa, huku taifa likikabiliwa na maafa''. Amelalamika Yatsenyuk.

Mlolongo wa changamoto

Kujiuzulu kwake kumekuja wakati Ukraine ikikabiliwa na changamoto ya kushughulikia mkasa wa ndege ya Malaysia iliyoangushwa katika eneo lake la mashariki, ambako wataalamu wa kimataifa wanafanya kazi ngumu ya kuchunguza jinsi ndege hiyo, MH17 ilivyodunguliwa, ikibeba watu 298.

Kudunguliwa kwa ndege ya Malaysia, MH17 mashariki mwa Urusi ni mojawapo ya changamoto zinazoikabili nchi hiyo kwa wahati huu.
Kudunguliwa kwa ndege ya Malaysia, MH17 mashariki mwa Urusi ni mojawapo ya changamoto zinazoikabili nchi hiyo kwa wahati huu.Picha: Reuters

Matatizo yanayoikumba nchi hiyo yalizidi kuongezeka jana baada ya Marekani kudai kwamba inao ushahidi kwamba wanajeshi wa Urusi walikuwa wakiishambulia Ukraine kwa mizinga wakiwa kwenye ardhi ya Urusi. Ingawa Serikali ya mjini Kiev na waasi wa mashariki wamekubali kusitisha mapigano karibu na mahali ilikoanguka ndege hiyo, milio ya silaha nzito iliendelea kusikika jana karibu na mji wa Donetsk, kilomita 60 tu kutoka eneo hilo la ajali.

Jeshi la Ukraine limesema kuwa maroketi yaliyorushwa kutoka ndani ya Urusi yalipiga maeneo karibu na uwanja wa ndege wa Luhansk, na sehemu mbali mbali katika mkoa wa Donetsk. Jeshi hilo pia lilidai kwamba ndege zake zilizodunguliwa Jumatano zilishambuliwa kutoka nchini Urusi, na kuongeza kuwa ingawa marubani wake waliruka salama kutoka ndani ya ndege hizo, bado hawajulikani waliko.

Ulaya yaiongezea vikwazo Urusi

Wakati huo huo Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limesema kinachoendelea mashariki mwa Ukraine ni vita vya wenyewe kwa wenyewe, na kuzitaka pande zote katika mgogoro huo kuheshimu mkataba wa Geneva. Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani Marie Harf ametoa tahadhari kwamba Urusi inajiandaa kuwapatia silaha nzito zaidi waasi wanaotaka kujitenga na Ukraine.

Kwa miezi kadhaa, Ukraine imekuwa ikipambana na waasi wa mashariki wanaotaka kujitenga.
Kwa miezi kadhaa, Ukraine imekuwa ikipambana na waasi wa mashariki wanaotaka kujitenga.Picha: Reuters

Huku hayo yakijiri Umoja wa Ulaya umesema umeongeza maafisa 15 wa Urusi na Ukraine pamoja na makampuni 18 kwenye orodha ya vikwazo, kama adhabu kwa Urusi kwa kuendelea kwake kuchochea ghasia mashariki mwa Ukraine. Hata hivyo, Uingereza na Ufaransa vimerushiana maneno makali, baada ya Uingereza kuukosoa uamuzi wa Ufaransa kuendelea na mpango wa kuiuzia Urusi meli za kisasa za kivita, licha ya tuhuma zinazoikabili.

Maafisa wa ulinzi wa Marekani wamesema kwamba Urusi inaendelea kuwarundika wanajeshi wake karibu na mpaka wake na Ukraine, hususan baada ya kuangushwa kwa ndege ya Malaysia katika eneo linalodhibitiwa na waasi wa mashariki mwa Ukraine.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/DPAE/APE

Mhariri: Josephat Charo