1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSomalia

Waziri wa ulinzi wa Somaliland ajiuzulu

9 Januari 2024

Waziri wa ulinzi wa Somaliland Abdiqani Mohamud Ateye amejiuzulu kupinga hatua ya serikali yake ya kutia saini makubaliano yanayoiruhusu Ethiopia kutumia bandari ya bahari ya Sham ya Berbera

https://p.dw.com/p/4b1HY
Rais wa Somaliland Muse Bihi Abdi awasili katika hafla ya kutia saini makubaliano na Ethiopia mnamo Januari 1, 2024
Rais wa Somaliland Muse Bihi AbdiPicha: TIKSA NEGERI/REUTERS

Ateye amesema katika mkutano wa awali na Rais wa Somaliland Muse Bihi Abdi, alielezea kuwa kwa kuruhusu wanajeshi wa Ethiopia kuwa na kambi katika ardhi ya Somaliland kimsingi ni hatua isiyofaa.

Ateye ameongeza kwamba alimuarifu Rais kuwa eneo linalopendekezwa kwa ujenzi wa kambi hiyo ya jeshi la wanamaji la Ethiopia kihaki linamilikiwa na jamii yake, lakini Rais huyo alipuuzilia mbali wasiwasi wake.

Soma pia:Rais wa Somalia afuta mkataba wa Somaliland na Ethiopia

Hata hivyo, hakukuwa na majibu ya haraka kutoka kwa serikali za Somaliland na Ethiopia kuhusiana na matamshi ya waziri huyo.

Wakati wa mahojiano na kituo kimoja cha televisheni siku ya Jumapili, Ateye alisema kuwa Ethiopia inasalia kuwa adui namba moja wa Somaliland.

Ateye amtuhumu Abiy kwa kujaribu kudhibiti eneo la Somaliland bila mazungumzo thabiti

Wiki iliyopita, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na Rais wa Somaliland, Muse Bihi Abdi, walitia saini makubaliano hayo ambayo yamefungua njia kwa Ethiopia kuendesha shughuli zake za baharini katika eneo hilo na kuiwezesha kukifikia kituo cha kijeshi kilichokodishwa kwenye Bahari ya Sham.

Ateye amemtuhumu Abiy kwa kujaribu kudhibiti eneo hilo bila mazungumzo thabiti.

Makubaliano yasababisha mgawanyiko miongoni mwa raia wa Somaliland

Makubaliano hayo yameibua maandamano kote jimboni Somaliland, huku wakaazi wakigawanyika kuhusiana na mkataba huo.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed akihudhuria mkutano wa waandishi wa habari katika ikulu ya Chigi mjini Rome, Italia mnamo Februari 6, 2023
Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: Massimo Percossi/Ansa/ZUMA Press/IMAGO

Baadhi wanaona uwezekano wa manufaa ya kiuchumi huku wengine wakihofia kuhatarisha uhuru wao.

Soma pia: Umoja wa Ulaya watia neno mkataba wa Ethiopia na Somaliland

Somalia imepinga makubaliano hayo na kuyataja kuwa tishio kwa uhuru wake kutoka kwa jimbo la Somaliland, ambalo lilijitenga nayo miongo kadhaa iliyopita lakini madai yake ya kuwa taifa huru hayatambuliwi kimataifa.

Ethiopia yafanya mazungumzo ya ushirikiano wa kijeshi na Somaliland

Ethiopia imesema Jumatatu kwamba imefanya mazungumzo ya ushirikiano wa kijeshi na Somaliland hii ikiwa ni wiki moja tu baada ya makubaliano yake na jimbo hilo linalojitawala kuzua mvutano katika Pembe ya Afrika.

Soma pia: Somalia yapinga makubaliano ya Ethiopia-Somaliland

Licha ya wasiwasi wa kikanda na kimataifa juu ya mkataba huo, mkuu wa jeshi hilo la Ethiopia Birhanu Jula alijadili ushirikiano wa kijeshi na mwenzake wa Somaliland Nuh Ismail Tani hapo jana Jumatatu. Haya ni kulingana na taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa kijamii wa Facebook na jeshi la Ethiopia.

Jamii ya kimataifa yatoa miito ya kuheshimiwa kwa uhuru wa Somalia

Mazungumzo hayo mjini Addis Ababa yamefanyika wakati ambapo Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud ameanza ziara katika taifa jirani la Eritrea.

Somalia inatafuta uungwaji mkono wa kimataifa kuhusu mkataba huo wenye utata wa Januari 1 kati ya Ethiopia na Somaliland.

Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Marekani zimetoa wito wa utulivu na heshima kwa uhuru na mamlaka ya taifa la Somalia.