1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Baraza la mawaziri Israel laidhinisha makubaliano

18 Januari 2025

Baraza la Mawaziri la Israel limeidhinisha mapema leo makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka ambao bado wanashikiliwa na Hamas. Ofisi ya Waziri Mkuu ya Israel imesema.

https://p.dw.com/p/4pJhN
Israel ITel Aviv 2025 |
Waandamanaji mjini Tel Aviv, Israel wakishinikiza kurejeshwa nyumbani kwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na HamasPicha: Jack Guez/AFP

Baraza la Mawaziri la Israel limeidhinisha mapema leo makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka ambao bado wanashikiliwa na Hamas. Ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu imesema hayo ikiwa ni siku moja tu kabla ya kuanza kwa makubaliano yaliyopangwa.

Katika kikao kilichofanyika kwa zaidi ya saa sita hatimaye serikali ya Israel iliridhia makubaliano hayo ambayo yanaweza kutengeneza njia ya kuvimaliza vita hivyo vilivyodumu kwa miezi 15. Katika awamu ya kwanza ya mpango huo, mapigano yatasitishwa kuanzia kesho mchana na kwa muda wa wiki sita. Hamas itawaachilia mateka 33 wa Israel, huku wafungwa karibu 2000 wa Kipalestina wakiachiliwa pia kutoka kwenye magereza ya Israel.

Soma zaidi. Baraza la mawaziri la Israel laidhinisha makubaliano ya kusitisha mapigano

Hata hivyo, Huko Gaza, ndege za kivita za Israel zimeendeleza mashambulizi makubwa tangu kutangazwa kwa mpango huo wa kusitishwa mapigano. Madaktari katika ukanda wa Gaza wamesema mashambulizi ya mapema leo yamewaua watu watano katika eneo la Mawasi na kufikisha idadi ya watu 119 waliouawa kwa mashambulio hayo ya mabomu tangu kutangazwa kwa makubaliano hayo siku ya Jumatano.