1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Kiarabu yalaani mashambulizi ya Israel, Rafah

Hawa Bihoga
27 Mei 2024

Mataifa kadhaa ya kiarabu yamelaani mashambulizi ya Israel yaliolenga mahema ya wakaazi karibu na mji wa kusini mwa Ukanda wa Gaza wa Rafah, wizara ya afya ya Gaza inayoongozwa na Hamas imesema watu kadhaa wameuwawa.

https://p.dw.com/p/4gKB0
Palestina, Rafah | Makaazi yalioharibiwa kwa mashambulizi ya anga ya Israel.
Baadhi ya makaazi ya Wapalestina yalioharibiwa vibaya na mashambulizi ya IsraelPicha: Abed Rahim Khatib/dpa/picture alliance

Miongoni mwa mataifa hayo ni pamoja na Misri na Qatar, katika taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Misri imelaani kile ilichokiita "mashambulizi ya makusudi ya vikosi vya Israel" kwa Wapalestina ambao wamekimbia mapigano katika maeneo mengine ya Gaza na kujiifadhi katika mji wa Rafah na kuongeza kuwa huo ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Qatar pia, ikilaani mashambulizi hayo ya Israel imerudia kusema kuwa huo ni "ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa" ambao utasababisha mzozo mkubwa wa kiutu katika Ukanda huo uliozingirwa na vikosi vya Israel.

Aidha Qatar imesema mashambulizi hayo yanaweza kuzorotesha juhudi zinazoendelea za upatanishi na kuzuia makubaliano juu ya usitishwaji wa kudumu wa mapigano na ubadilishanaji wa mateka.

Idara ya ulinzi wa umma ya Gaza imesema siku ya Jumatatu kwamba, idadi ya waliokufa kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel kwenye kambi ya raia imeongezeka hadi watu arobaini.

Soma pia:Mataifa ya kiarabu yahofia uhamisho mpya wa Wapalestina

Wizara ya afya ya Gaza pia ilio chini ya Hamas, ikitoa taarifa sawia na hiyo imeongeza kuwa idadi kubwa ya miili ya watu "imeteketea" kutokana na mashambulizi hayo.

Baadhi ya Wapalestina wamesema kwamba mashambulizi ya Israel yamesababisha hasara kubwa katika eneo la Ukanda wa Gaza na kuwataka washirika wake kujitafakari upya wakizingatia maelfu ya watu waliopeteza maisha tangu kuzuka kwa vita hivyo. 

"Rais Biden ambae alidai anataka mapigano yasitishwe... Wanataka kuuwa watu wa Gaza. Watu wasio na hatia, watu thabiti. Tutaendelea kubaki imara." Alisema Mohammed Al-Attar ni mkaazi wa Gaza.

Mohammed aliongeza kwamba "haijalishi tutapoteza mashahidi kiasi gani, Mungu akipenda tutaendelea kuwa imara."

UNRWA: Gaza inashuhudia mauaji ya "kutisha" Rafah

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi wa Palestina UNRWA, linasema kwamba mashambulizi ya Israel dhidi ya familia zinazotafuta hifadhi huko Rafah katika ncha ya kusini mwa Ukanda wa Gaza ni "ya kutisha".

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza

Shirika hilo limeongeza kuwa wengi waliojeruhiwa ni watoto na wanawake miongoni mwa wale waliouwawa, huku wakifananisha eneo hilo na "kuzimu."

Israel imesema vikosi vyake vya anga vilishambulia kambi ya Hamas.

Soma pia:Vita vya Gaza: Blinken afanya mazungumzo na Netanyahu

Hata hivyo kufuatia jeshi la Israel kushutumiwa kushambulia mahema ya raia kwenye mashambulizi hayo na kuuwa watu kadhaa kwa mujibu wa mamlaka ya ndani ya Gaza limesema kwamba wanafanya uchunguzi "yakini"

Katika hatua nyingine Israel imeuamuru Ubalozi mdogo wa Uhispania mjini Jerusalem kuacha kutoa huduma za kibalozi kwa Wapalestina kuanzia Juni 1, ikiwa ni hatua ya kujibu uamuzi wa serikali mjini Madrid ya kulitambua taifa la Palestina.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imesema kuwa maagizo hayo yataanza kutekelezwa mara moja kuanzia Juni mosi.