Mustakabali wa Haiti mashakani baada ya mauaji ya rais
8 Julai 2021Haiti iliyokuwa ikijpambana na yenye machafuko imetumbukia katika mustakabali wa mashaka baada ya kuuawa kwa Rais Jovenel Moise, kulikofuatiwa na mapigano ya risasi ambamo mamlaka ilisema polisi waliwaua washukiwa saba, kuwatia mbaroni wengine sita na kuwaokoa maafisa watatu waliokuwa wanashikiliwa mateka.
Maafisa waliahidi kuwakamata wote waliohusika na uvamizi wa alfajiri nyumbani kwa Moise mapema Jumatano ambapo rais alipigwa risasi na kufariki na mkewe, Martine, akijeruhiwa vibaya. Alisafirishwa kwenda Miami kwa matibabu.
"Msako dhidi ya mamluki unaendelea," Leon Charles, mkurugenzi wa Polisi ya Kitaifa ya Haiti, alisema Jumatano usiku wakati akitangaza kukamatwa kwa washukiwa. "Hatima yao imedhamiriwa: Watauawa kwenye mapigano au watakamatwa."
Siku ya Alhamisi, Charles aliiambia Radio Metropole kwamba jumla ya washukiwa sita wamekamatwa na saba wameuawa na kwamba polisi bado wanatafuta wengine zaidi.
Maafisa hawakutoa maelezo yoyote juu ya washukiwa, pamoja na mataifa yao, wala hawakuzungumzia nia au kusema ni nini kiliwaongoza polisi kwao. Walisema tu kwamba shambulio hilo lililolaaniwa na vyama vikuu vya upinzani vya Haiti na jumuiya ya kimataifa lilitekelezwa na "kikundi kilichofunzwa sana na chenye silaha nyingi," ambacho wanachama wake walizungumza Kihispania au Kiingereza.
Soma pia: Rais wa Haiti auwawa kinyama nyumbani kwake
Waziri Mkuu Claude Joseph alichukua uongozi wa Haiti kwa msaada wa polisi na jeshi, na kutangaza hali ya dharura ya wiki mbili kufuatia mauaji ya Moise, ambayo yalilishtua taifa linalokabiliana na viwango vya juu kabisaa vya umaskini katika ulimwengu wa magharibi, vurugu kuyumba kisiasa.
Mfumuko wa bei na vurugu za magenge vimeongezeka zaidi wakati chakula na mafuta vikizidi kukosekana katika nchi ambayo asilimia 60 ya Wahaiti wanapata chini ya $ 2 kwa siku. Hali hii inayozidi kuwa mbaya inakuja wakati Haiti bado inajaribu kupona kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea mwaka 2010 na Kimbunga Matthew mwaka 2016, achilia mbali historia ya udikteta na machafuko ya kisiasa.
"Kuna ombwe hili sasa, na wanahofia nini kitatokea kwa wapendwa wao," alisema Marlene Bastien, mkurugenzi mtendaji wa wa Family Action Network Movement, ambalo ni shirika linalosaidia watu katika jamii ndogo ya Wahaiti mjini Miami.
Alisema ni muhimu kwa utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden kuchukua jukumu kubwa zaidi katika kusaidia juhudi za mazungumzo ya kitaifa nchini Haiti kwa lengo la kufanya uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika.
Bastien alisema pia anataka kuona ushiriki wa Wahaiti waishio ng'ambo: "Hakuna suluhisho la haraka. Watu wa Haiti wamekuwa wakilia na kuteseka kwa muda mrefu. "
Soma pia: Washukiwa 4 wa mauji ya rais wauwawa Haiti.
Haiti ilikua inazidi kutokuwa na utulivu chini ya Moise, ambaye alikuwa akitawala kwa amri kwa zaidi ya mwaka mmoja na alikabiliwa na maandamano ya vurugu wakati wakosoaji walimshtumu kwa kujaribu kujiongezea mamlaka wakati upinzani ulimtaka aondoke.
Kulingana na katiba ya Haiti, nafasi ya Moise inapaswa kuchukuliwa na rais wa Mahakama Kuu ya Haiti, lakini jaji mkuu alikufa mnamo siku za hivi karibuni kutokana na COVID-19, ikiacha wazi swali la nani ana haki ya kurithi nafasi hiyo.
Ariel Henry asema yeye ndiye waziri mkuu halali
Joseph, wakati huo huo, alipaswa kurthiwa na Ariel Henry, daktari wa neva ambaye aliteuliwa kuwa waziri mkuu na Moise siku moja kabla ya mauaji.
Henry aliliambia shirika la habari la Associated Press katika mahojiano mafupi kwamba yeye ndiye waziri mkuu, akiitaja hali iliyojitokeza kuwa ya kipekee na ya kutatanisha. Katika mahojiano mengine na Redio Zenith, alisema hakuwa na mzozo wowote na Joseph. "Sikubaliani tu na ukweli kwamba watu wamechukua maamuzi ya haraka ... wakati ambapo wakati unahitaji utulivu zaidi na kukomaa," alisema.
Soma pia: Rais wa Haiti Jovenel asema hatajiuzulu
Moise alikuwa amekabiliwa na maandamano makubwa katika miezi ya hivi karibuni ambayo yalibadilika kuwa ghasia wakati viongozi wa upinzani na wafuasi wao walipokataa mipango yake ya kufanya kura ya maoni ya kikatiba na mapendekezo ambayo yangeiongezea mamlaka nafasi ya urais.
Siku ya Alhamisi, usafiri wa umma na wachuuzi wa mitaani viliadimika, katika hali isiyo ya kawaida kwa barabara za mji mkuu Port-au-Prince, ambazo kawaida hufurika watu.
Marco Destin, 39, alikuwa akitembea kwenda kuiona familia yake kwani hakuwa mabasi, yanayojulikana kama tap-tap. Alikuwa amewabebea mkate kwa sababu walikuwa hawajatoka nyumbani kwao tangu mauaji ya rais kwa kuhofia maisha yao. "Kila mtu nyumbani analala na jicho moja wazi na jicho lingine limefumba, "alisema. "Ikiwa mkuu wa nchi hajalindwa, sina ulinzi wowote ule. "
Destin alisema Haiti daima imekuwa nchi ngumu na hivyo hakuwa na uhakika ni nini siku za usoni zingeleta. "Haiti haijui ni mwelekeo gani inachukua sasa hivi, "alisema." Kusema kweli, sijui suluhisho ni nini. Kumekuwa na mapambano ya kuwania madaraka siku zote."
pigania nguvu. "
Risasi zilirindima mara kwa mara katika jiji lote saa kadhaa baada ya mauaji, ukumbusho mbaya wa nguvu inayoongezeka ya magenge ambayo yaliwakosesha makazi watu zaidi ya 14,700 mwezi uliopita pekee baada ya kuziketeza na kuzipora nyumba zao katika mapambano ya kuwania maeneo.
Soma pia:Tetemeko kubwa la ardhi laikumba Haiti
Robert Fatton, mtaalam wa siasa wa Haiti katika Chuo Kikuu cha Virginia, alisema magenge yalikuwa nguvu ya kushindana nayo na sio kwamba vikosi vya usalama vya Haiti vinaweza kutekeleza hali ya mzingiro.
"Kwa kweli ni hali ya mlipuko," alisema na kuongeza kuwa kuna uwezekano wa uingiliaji wa kigeni kwa aina fulani ya uwepo wa jeshi la Umoja wa Mataifa. "Iwapo Claude Joseph ataweza kukaa madarakani ni swali kubwa. Itakuwa ngumu sana kufanya hivyo ikiwa hataunda serikali ya umoja wa kitaifa. "
Joseph aliiambia AP kwamba anaunga mkono uchunguzi wa kimataifa kuhusu mauaji hayo na anaamini uchaguzi uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huu unapaswa kufanywa, kwani aliahidi kufanya kazi na washirika wa Moise na wapinzani sawa.
"Kila kitu kiko chini ya udhibiti," alisema.
Chanzo: APE