Trump amtemea cheche Bi May kwa nyaraka zilizovuja
9 Julai 2019
Mzizi wa fitina katika mvutano unaoshuhudiwa baina ya Uingereza na Ikulu ya Rais Donald Trump mjini Washington, ni kuvuja kwa mlolongo wa mawasiliano ya kidiplomasia kutoka kwa balozi wa Uingereza nchini Marekani Kim Darroch, ambaye miongoni mwa tathmini kali alizozifanya kuhusu utawala wa Trump, alisema utawala huo umeparaganyika, na hauna uelekevu.
Soma zaidi: Trump aanza ziara rasmi nchini Uingereza
Balozi huyo alitilia shaka uwezo wa Trump hatimaye kuufanya utawala wake kuwa wenye kufuata utaratibu wa kawaida, wala kumaliza mifarakano ya ndani.
Undani wa mawasiliano hayo ulichapishwa katika toleo la Jumapili la gazeti la Mail on Sunday la nchini Uingereza, mwezi mmoja tu baada ya Trump kufanya ziara rasmi nchini humo.
London yamuunga mkono balozi wake
Serikali mjini London ilithibitisha uhalisia wa taarifa hizo, na kumtetea balozi Darroch kuwa alichokifanya kilikuwa katika mipaka ya majukumu yake, huku ukiapa kutumia uwezo wote kumtafuta aliyezivujisha ili aadabishwe kwa mujibu wa sheria.
Kumpata mvujishaji sio kazi rahisi, kwani kwa mujibu wa gazeti la Daily Telegraph, watu wapatao 100 katika wizara ya mambo ya nje wanaweza kuona mawasiliano hayo ya kibalozi yenye unyeti wa hali ya juu.
Soma zaidi: Uingereza yakasirishwa Marekani kuvujisha taarifa
Lakini wakati Uingereza ikijaribu kunusuru kile kinachojulikana kama ''uhusiano maalum'' kati yake na Marekani, mjini Washington rais Trump hakuweza kuficha hasira zake.
Kupitia mtandao wake wa twitter hapo jana alimshambulia vikali balozi Kim Darroch, akimtaja kuwa mtu asiejulikana wala kupendwa na kuheshimiwa nchini Marekani. Trump alisema hatakuwa na mahusiano yoyote ya kikazi na balozi huyo tena.
Trump amuandama Theresa May
Lakini Trump hakuishia kwa balozi huyo, bali alimlenga waziri mkuu wa Uingereza anayeondoka, Bi Theresa May, akisema alipuuza ushauri wake kuhusu kuuendesha mchakato wa Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya, maarufu kama Brexit, na kuamua kufuata mtazamo tofauti ambao kwa mujibu Trump, matokeo yake yamekuwa balaa tupu.
Kama kijembe kingine cha wazi kwa Theresa May, Trump alirejelea ziara aliyoifanya nchini Uingereza, na kuongeza kuwa kitu pekee anachoonea fahari ni kupokelewa na Malkia Elisabeth II.
Mvutano huu sio habari njema kwa matumaini ya Uingereza ya kupata makubaliano ya kibiashara na Marekani, baada ya kuondoka katika Umoja wa Ulaya.
afpe, ape