Iran yalaani uchunguzi wa Baraza la Haki za Binaadamu la UN
25 Novemba 2022Tehran ilikuwa imepinga kufanyika kwa kikao cha dharura cha baraza hilo siku ya Alhamisi kama ilivyoombwa na Ujerumani na Iceland. Ilikataa kabisa azimio ambalo lilipitishwa Ijumaa hii la kuanzishwa tume ya kutafuta ukweli kwa matukio ya ukandamizaji dhidi ya waandamanaji nchini Iran.
Iran imeshuhudia maandamano kwa zaidi ya miezi miwili yaliyochochewa na kifo cha mwanamke mwenye umri wa miaka 22 raia wa Kikurdi Mahsa Amini. Alikuwa amekamatwa kwa madai ya kukiuka sheria kali za mavazi ya wanawake nchini humo.
Soma zaidi: UN yaitaka Iran kusitisha kamatakamata ya waandamanaji
Maafisa wa serikali wameyashutumu mataifa ya kigeni kwa kuchochea machafuko hayo ambayo yanachukuliwa kama uvunjaji wa sheria. Wizara ya mambo ya nje ilisema Iran tayari imeunda tume ya kitaifa ya uchunguzi inayowahusisha wataalamu wa sheria na "wawakilishi huru".
Taarifa ya Wizara hiyo imebaini kuwa kuundwa kwa utaratibu wowote mpya wa kuchunguza matukio ya miezi miwili iliyopita nchini Iran ni kazi bure na inamaanisha ukiukaji wa mamlaka ya kitaifa ya nchi hiyo ya Kiislamu.
Tehran yapinga azimio hilo
Iran imesema "haiutambui ujumbe huo". Idadi kubwa kuliko ilivyotarajiwa ya baraza hilo lenye wanachama 47 waliunga mkono kuanzishwa kwa uchunguzi huo. Nchi 25 zilipiga kura ya Ndio, nchi 16 zilijizuia kupiga kura huku nchi 6 pekee ambazo ni Armenia, China, Cuba, Eritrea, Pakistan na Venezuela zikipinga hatua hiyo.
Soma zaidi: Umoja wa Mataifa walaani ukandamizaji wa Iran
Tehran iliishutumu Ujerumani na nchi nyingine ambazo ziliunga mkono azimio hilo kwa kutoa "madai ya uwongo na ya uchochezi kuhusu ukiukaji wa haki za wanaume, wanawake na watoto, madai ambayo Iran inayakanusha.
Wizara ya mambo ya nje ya Iran imedai kuwa azimio hili lilitolewa kwa shinikizo kutoka kwa makundi fulani ya kisiasa ambayo yanategemea habari za uongo zinazoenezwa na vyombo vya habari vinavyoipinga Iran.
Soma zaidi: Iran yazishutumu nchi za kigeni kwa machafuko yanayoendelea
Iran imeshutumu na kusema ni kosa la kimkakati la Ujerumani na nchi fulani za Magharibi na kwamba "upofu huo utakuwa na madhara kwa maslahi yao".
Wakati wa kikao cha Alhamisi, mkuu wa haki za Umoja wa Mataifa Volker Turk alisisitiza kuwa matumizi ya nguvu yasiyo ya lazima na yasiyo na usawa lazima yakomeshwe.
Turk alisema zaidi ya watu 300 wameuawa tangu kifo cha Amini na aliwaambia waandishi wa habari kwamba alijitolea kuitembelea Iran lakini hakupata jibu kutoka Tehran.